Ijumaa 17 Julai 2026 - 15:00
Kubeba Vifaa vya Kidini Kwapigwa Marufuku Katika Magereza ya Bahrain

Hawza/ Kwa mtazamo wa kila anayefuatilia masuala ya Bahrain, imekuwa wazi kuwa utawala wa Aal Khalifa umejengwa juu ya msingi wa ubaguzi na mateso ya kidini. Serikali hiyo hutoa madai yasiyoendana na uhalisia, husambaza simulizi za uongo kuhusu ustahimilivu na kuishi pamoja kwa amani, kisha huanza kuziamini yenyewe na kuzifanyia kazi kana kwamba wengine pia wanaziamini.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Mir'at al-Bahrain, magereza na vituo vinavyo washikilia wafungwa wa kisiasa ndio ushahidi mkubwa unaobatilisha propaganda zote za utawala. Humo husimuliwa visa vingi vya unyanyasaji unaochochewa na misingi ya kimadhehebu pamoja na kunyimwa haki za msingi ambazo serikali na taasisi zake, hususan Wizara ya Mambo ya Ndani, hudai kwa uongo kuwa zinazilinda na kuzihakikisha.

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa kutoka Gereza la Al-Hawd al-Jaf zinaonesha kuwa wafungwa wananyimwa mahitaji ambayo kwa mujibu wa sheria ni haki zao gerezani, yaani vifaa vya kidini vinavyohitajika na wafungwa wa Kishia kwa ajili ya kutekeleza ibada zao za kidini.

Mwanaharakati wa haki za binadamu Ibtisam Al-Sayegh alitangaza kuwa; kulikuwa na juhudi za kuwapatia wafungwa mahitaji hayo, ikiwemo Qur'ani Tukufu na vitabu vya dua. Hata hivyo, juhudi hizo zilikataliwa mara moja na mamlaka husika. Al-Sayegh alisema amepokea simu nyingi kutoka kwa wafungwa wakihitaji vifaa hivyo, jambo linaloonesha kuwa kunyimwa huko ni hali halisi, si madai yasiyo na msingi.

Ushuhuda wa mmoja wa wafungwa wa zamani pia unathibitisha kauli za Al-Sayegh, alisema kuwa; uongozi wa Gereza la Al-Hawd al-Jaf unazuia kuingizwa kwa turbah na vitabu vya dua, hali inayowalazimu wafungwa kutumia vipande vya karatasi ngumu wakati wa kusujudu.

Kwa msingi huo, matukio haya hayawezi kuchukuliwa kuwa ni hatua za kawaida za kiutawala, bali ni ukiukaji unaolenga kiini cha haki ya uhuru wa dini na imani. Viwango vya kimataifa, hususan Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa pamoja na Kanuni za Kiwango cha Chini za Umoja wa Mataifa kuhusu Matibabu ya Wafungwa (Kanuni za Nelson Mandela), vinasisitiza haki ya watu waliopokonywa uhuru wao kutekeleza ibada zao za kidini na kupata vitabu pamoja na vifaa vinavyohitajika kwa ajili hiyo, isipokuwa pale ambapo kuna sababu halali na zinazoweza kuthibitishwa za kiusalama.

Marufuku ya jumla dhidi ya Qur'ani Tukufu, vitabu vya dua na turbah, kwa mujibu wa ripoti hiyo, inaonekana kuwa ni mwendelezo wa sera ya kibaguzi inayolenga utambulisho maalumu wa kidini.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa, yanayotokea ndani ya magereza hayawezi kutenganishwa na hali ya jumla ya Bahrain katika miezi ya hivi karibuni. Shinikizo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia halijabaki tena ndani ya magereza pekee, bali limekuwa la kimfumo na sasa limeenea hadi katika maisha ya umma. Tangu kuanza kwa msimu wa Ashura (Mwezi wa Muharram), kumekuwa na maagizo rasmi na vizuizi mbalimbali dhidi ya Husayniyyah na shughuli za ibada. Aidha, kumeshuhudiwa wimbi la kuitwa kwa mahojiano, uchunguzi na kukamatwa idadi ya wanazuoni, makhatibu na waombolezaji (madahi), hali inayodhihirisha kuendelea kwa mtazamo wa kiusalama katika kushughulikia ibada za kidini badala ya kuzitambua kuwa ni haki ya msingi iliyolindwa na mikataba ya kimataifa.

Kwa kuzingatia hali hiyo, viashiria vya haki za binadamu, iwe katika nyanja ya uhuru wa kuamini au uhuru wa kutekeleza ibada, vinatoa taswira wazi ya sera inayolenga haki za kidini za sehemu kubwa ya raia wa Bahrain.

Kutokana na hayo, ripoti hiyo inasema kuwa; taasisi za Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu zinalazimika kushughulikia ukiukaji huu si kama makosa ya kiutawala yaliyojitenga, bali kama sehemu ya faili la ubaguzi wa kidini wa kimfumo nchini Bahrain, hususan wakati ambao mamlaka za nchi hiyo zinaendelea kuyakanusha matukio hayo ilhali ushahidi na shuhuda zinazoongezeka kila siku zinapingana wazi na simulizi rasmi la serikali.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha